![]() |
Mbaraka Mwinshehe Mwaruka |
Mbaraka
Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro 27 Juni, 1944. Mbaraka Mwinshehe
alikuwa mtoto wa pili kuzaliwa katika watoto 12 . Baba yake Mzee Mwinshehe
Mwaruka alikuwa Mluguru msomi na karani katika mashamba ya katani, na mama yake
alikuwa Mngoni. Kati ya watoto hao kumi na mbili, ni yeye na wadogo zake Zanda
na Matata ndio waliweza kuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia
nyimbo za kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum pia
bendi hiyohiyo. Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa
kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga (Kisarawe) akawe chifu wa huko
na wakoloni. Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo
baba yake Mbaraka, Mzee Mwaruka. Mbaraka alisoma mpaka kidato cha tatu na kuacha
shule ili awe mwanamuziki.
Mbaraka
Mwinshehe alianza kushiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa
shule, wakati huo alipenda kupiga sana filimbi katika mtindo wa ‘kwela’, mtindo
huu ulitoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji maarufu kama Spokes Mashiyan,
na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na makundi mengi ya jiving
yalikuweko katika shule za sekondari. Jiving ilikuwa ni mtindo wa kundi kuimba
na kucheza kwa ‘steps’zilizoigwa kutoka kwa wasanii wa Afrika ya Kusini.
Mbaraka
alikuwa akishiriki kupiga filimbi wakati wa wikiendi kwenye maonyesho ya
Morogoro Jazz Band wakati huo akiwa bado shule. Siku moja kwenye mwaka 1965,
wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao, Mbaraka
alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa
kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta
maisha , walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake.
Kesho yake
wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa
wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga rhythm
walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm,
akakubali. Wakati huo ni wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee
waliokuwa wanalipwa mshahara kwa mwezi, wengine wote walipata posho kidogo kila
lilipopigwa dansi. Siku moja walialikwa Dar Es Salaam kwa ajili ya mashindano
na Kilwa Jazz, kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi,
wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye
alikuwa akilipwa shilingi 150 akagoma kwenda Dar kwa kusisitiza kuwa mpiga
rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda
Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao
walikuwa wakienda bila mpiga solo.
Mbaraka
alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda.
Akapandishwa mshahara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu
sana, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake
Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo mkuu wa Morogoro Jazz Band.
![]() |
Mbaraka akiwa amefuga ndevu kumfuatia Franco Luambo aliyeanza kufuga ndevu wakati guo |
Upigaji wake
wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anaetaka kujiendeleza katika upigaji wa
gitaa la solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super
Volcano alipitia staili nyingi za upigaji wa gitaa lake la solo, baadhi ya
staili za bendi ya Morogoro kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika,
zote zilionyesha upigaji tofauti kwa mtindo, haikuwa kubadili jina tu la
staili. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili
muziki wenyewe. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za
Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki walikuwa wakienda Morogoro
kufaidi wiki endi ya muziki kutoka kwa aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro
Jazz.
![]() |
Binti ya Mbaraka, Taji Mbaraka ambaye naye ni mwanamuziki muimbaji na mpiga bezi |
Siku ya
Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikiska kwa simanzi baada ya
kusikika kifo cha Mbaraka Mwinshehe, mpiga gitaa muimbaji, mtunzi na kiongozi
wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga kila wilaya ya
nchini Tanzania. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa
kuwa nguli huyu alifia katika hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya
muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari.
Kwa maelezo
ya Zebedee Japhet Kinoka au maarufu kama Super Zex mwanamuziki mkongwe, siku ya
tarehe 12 Januari 1979 alikuwa anatoka maeneo ya Kisauni kumtembelea Mtanzania
mwenzake aliyekuwa na hoteli huko, ambaye pia walitoka kijiji kimoja Maramba
huko Tanga. Anasema alipofika karibu na kanisa la Kongoya aliona gari aina ya
Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar na kwa spidi kali ikaenda na
kuligonga lori moja lililokuwa likitokea upande mwingine.
Ilikuwa
mchana kiasi kama saa 7 hivi. Watu wakakimbilia kungalia ajali akiwemo yeye. Na
mara moja akamtambua Mbaraka na kuwambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki
Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinshehe. Katika gari lile kulikuweko watu watatu
Mbaraka alikuwa amekaa mbele pamoja na dereva. Dereva (maelezo ya baadaye
yalimtambua dreva huyo kuwa alikuwa rafiki wa Mbaraka na mkazi wa Moshi aliitwa
Omari Abdi, kuna maelezo mengine kuwa Abdi pia alikuja fia hospitalini si pale
kwenye ajali) na abiria aliyekuwa nyuma alikufa palepale, ikalazimika kuanza
kukata mabati ili kumuondoa Mbaraka aliyekuwa amebanwa miguu katika gari lile
lililoharibika, yeye alikuwa bado hai.
Wakati kazi
hiyo inaendelea Zebedee alikimbilia Kengeleni Bar ambapo Jamhuri Jazz Band
(Bendi ya Watanzania) ilikuwa ikipiga muziki na kuwambia kuwa mwenzao kaumia
sana, nao wakatoka mbio, wakiwemo akina Harrisson Siwale. Mbaraka aliweza
kutolewa kwenye gari na kupelekwa kwenye hospitali ya Makadara. Zebedee pia
akatumwa kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo
walikuwa wakipiga Zambia Bar, wanamuziki walipofika hospitali wakaambia watoe
damu na wakaanza kukwepa kutoa damu kwa visingizio mbalimbali.
Muda si
mrefu Mbaraka Mwinyshehe akafariki. Mbaraka alifarika 12 Januari 1979 akiwa na
umri mdogo wa miaka 34 tu. Kwa kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa
umefungwa wakati huo kutokana na mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili,
mwili wa Mbaraka alisafirishwa mpaka mpakani na kupokelewa na ndugu marafiki na
Maafisa wa Wizara ya Utamaduni.
Mbaraka
Mwinyshehe alizikwa Mzenga Kisarawe
No comments