MIAKA 39 BILA MBARAKA MWINSHEHE


Mbaraka Mwinshehe Mwaruka
Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro 27 Juni, 1944. Mbaraka Mwinshehe alikuwa mtoto wa pili kuzaliwa katika watoto 12 . Baba yake Mzee Mwinshehe Mwaruka alikuwa Mluguru msomi na karani katika mashamba ya katani, na mama yake alikuwa Mngoni. Kati ya watoto hao kumi na mbili, ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio waliweza kuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia nyimbo za kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum pia bendi hiyohiyo. Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga (Kisarawe) akawe chifu wa huko na wakoloni. Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo baba yake Mbaraka, Mzee Mwaruka. Mbaraka alisoma mpaka kidato cha tatu na kuacha shule ili awe mwanamuziki.
Mbaraka Mwinshehe alianza kushiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa shule, wakati huo alipenda kupiga sana filimbi katika mtindo wa ‘kwela’, mtindo huu ulitoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji maarufu kama Spokes Mashiyan, na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na makundi mengi ya jiving yalikuweko katika shule za sekondari. Jiving ilikuwa ni mtindo wa kundi kuimba na kucheza kwa ‘steps’zilizoigwa kutoka kwa wasanii wa Afrika ya Kusini.
Mbaraka alikuwa akishiriki kupiga filimbi wakati wa wikiendi kwenye maonyesho ya Morogoro Jazz Band wakati huo akiwa bado shule. Siku moja kwenye mwaka 1965, wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao, Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta maisha , walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake.
Kesho yake wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga rhythm walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm, akakubali. Wakati huo ni wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee waliokuwa wanalipwa mshahara kwa mwezi, wengine wote walipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi. Siku moja walialikwa Dar Es Salaam kwa ajili ya mashindano na Kilwa Jazz, kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa shilingi 150 akagoma kwenda Dar kwa kusisitiza kuwa mpiga rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo.
Mbaraka alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda. Akapandishwa mshahara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo mkuu wa Morogoro Jazz Band.
Mbaraka akiwa amefuga ndevu kumfuatia Franco Luambo aliyeanza kufuga ndevu wakati guo
Upigaji wake wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anaetaka kujiendeleza katika upigaji wa gitaa la solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za upigaji wa gitaa lake la solo, baadhi ya staili za bendi ya Morogoro kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika, zote zilionyesha upigaji tofauti kwa mtindo, haikuwa kubadili jina tu la staili. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki walikuwa wakienda Morogoro kufaidi wiki endi ya muziki kutoka kwa aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro Jazz.
Binti ya Mbaraka, Taji Mbaraka ambaye naye ni mwanamuziki muimbaji na mpiga bezi
Siku ya Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikiska kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha Mbaraka Mwinshehe, mpiga gitaa muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga kila wilaya ya nchini Tanzania. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia katika hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari.
Kwa maelezo ya Zebedee Japhet Kinoka au maarufu kama Super Zex mwanamuziki mkongwe, siku ya tarehe 12 Januari 1979 alikuwa anatoka maeneo ya Kisauni kumtembelea Mtanzania mwenzake aliyekuwa na hoteli huko, ambaye pia walitoka kijiji kimoja Maramba huko Tanga. Anasema alipofika karibu na kanisa la Kongoya aliona gari aina ya Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar na kwa spidi kali ikaenda na kuligonga lori moja lililokuwa likitokea upande mwingine.
Ilikuwa mchana kiasi kama saa 7 hivi. Watu wakakimbilia kungalia ajali akiwemo yeye. Na mara moja akamtambua Mbaraka na kuwambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinshehe. Katika gari lile kulikuweko watu watatu Mbaraka alikuwa amekaa mbele pamoja na dereva. Dereva (maelezo ya baadaye yalimtambua dreva huyo kuwa alikuwa rafiki wa Mbaraka na mkazi wa Moshi aliitwa Omari Abdi, kuna maelezo mengine kuwa Abdi pia alikuja fia hospitalini si pale kwenye ajali) na abiria aliyekuwa nyuma alikufa palepale, ikalazimika kuanza kukata mabati ili kumuondoa Mbaraka aliyekuwa amebanwa miguu katika gari lile lililoharibika, yeye alikuwa bado hai.
Wakati kazi hiyo inaendelea Zebedee alikimbilia Kengeleni Bar ambapo Jamhuri Jazz Band (Bendi ya Watanzania) ilikuwa ikipiga muziki na kuwambia kuwa mwenzao kaumia sana, nao wakatoka mbio, wakiwemo akina Harrisson Siwale. Mbaraka aliweza kutolewa kwenye gari na kupelekwa kwenye hospitali ya Makadara. Zebedee pia akatumwa kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wakipiga Zambia Bar, wanamuziki walipofika hospitali wakaambia watoe damu na wakaanza kukwepa kutoa damu kwa visingizio mbalimbali.
Muda si mrefu Mbaraka Mwinyshehe akafariki. Mbaraka alifarika 12 Januari 1979 akiwa na umri mdogo wa miaka 34 tu. Kwa kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa umefungwa wakati huo kutokana na mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili, mwili wa Mbaraka alisafirishwa mpaka mpakani na kupokelewa na ndugu marafiki na Maafisa wa Wizara ya Utamaduni.
Mbaraka Mwinyshehe alizikwa Mzenga Kisarawe

 
Kaburi la Mbaraka Mwinshehe

No comments

ANANIA NGOLIGA AND JOHN KITIME RELEASE THEIR 1ST ALBUM

THE  songs in this 10-song album, are a variety of songs composed by the duo, played in their own unique style. Anania Ngoliga of the  Wagog...